MOURINHO: MLIYEMUONA MAN UTD SIO RADAMEL FALCAO

Thursday, 11 June 2015



Meneja wa Chelsea Jose Mourinho anasema "Inamuuma" kuona watu wa soka la Kiingereza hawajashuhudia makali ya mshambuliaji mahili wa kimataifa wa Colombia Radamel Falcao, na hivyo ana mpango wa kumsaidia mchezaji huyo kurudisha makali yake katika kuzitingisha nyavu za wapinzani.

Radamel Falcao alijiunga na klabu ya Manchester United kwa mkopo msimu uliokwisha akitokea klabu ya Monaco lakini tangu ajiunge na klabu hiyo hajaonesha makali kama ilivyotegemewa na hivyo klabu hiyo ina mpango wa kuachana naye.

Jose Mourinho ametoa fursa ya kumsaidia mchezaji huyo kurudi katika kiwango chake cha awali kama atajiunga na klabu ya Chelsea iliyotwaa Ubingwa wa Ligi msimu ulioisha.

Mtandao wa Goal ulitoa taarifa mwanzoni mwa mwezi Juni kwamba Mourinho amekuwa msukumo mkubwa katika klabu hiyo kuhusiana na Falcao kujiunga na miamba hao akiwa na imani ya kurejesha kiwango cha mshambuliaji huyo kama alivyokuwa katika klabu za Porto ya Ureno na Atletico Madrid ya Hispania.

Sasa Kocha huyo Jose Mourinho ameuthibitishia umma kupitia DirecTv Sports kwamba,"Ni kweli inauma sana kwamba watu nchini Uingereza wanaamini kwamba waliyemuona Manchester United ndiye Falcao"

"Ni mchezaji ninayemfahamu, mchezaji ambaye nimekuwa nikimfuatilia tangu akiwa na klabu ya Atletico Madrid na kama ninaweza kumsaidia Falcao kurudi katika ubora wake nitafanya hivyo."

Falcao ana nia ya kuendelea kubaki na kukipiga katika ligi hiyo bora barani Ulaya na anataka kujiunga na Mourinho Stamford Bridge baada ya kutimka Manchester United.

Baada ya mshambuliaji huyo kushindwa kuwika mbele ya kocha Louis Van Gaal, klabu ya Manchester United haikutaka tena kuchukua uamuzi wa kumnunua mchezaji huyo aliyekuwa klabuni hapo kwa mkopo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 aliifungia klabu hiyo jumla ya magoli manne tu katika michezo 26 ya ligi kuu aliyoshiriki na iliripotiwa kwamba uhusiano wake na kocha Van Gaal katikati ya msimu haukuwa mzuri.

0 comments:

Post a Comment