BAADA YA KUIGALAGAZA CHELSEA MWAKA 2012, SASA ATUA RASMI KLABUNI HAPO...

Friday, 3 July 2015




Klabu ya Chelsea na Monaco zimekubaliana vigezo vya uhamisho wa mkopo wa mshambuliaji Radamel Falcao.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia ambaye alisajiliwa kwa ada ya pauni milioni 50 kutoka Ligue 1 mwaka 2013, atakaa na klabu ya chelsea kwa msimu wa 2015-2016.

Kiungo chipukizi wa Chelsea Mario Pasalic, mwenye umri wa miaka 20 atajiunga na klabu ya Monaco kwa mkopo kama sehemu ya makubaliano yao.

"Nina furaha sana kujiunga na Chelsea na siwezi kusubiri kuanza mazoezi na kutoa msaada katika kusudio letu la kuulinda ubingwa wa Ligi na kuwa na mafanikio Ulaya." Falcao aliiambia tovuti rasmi ya klabu.

Goal ilitanabaisha mwezi uliopita kwamba Jose Mourinho alikuwa akitoa msukumo kwa Chelsea kumuwania Falcao, ambaye ana mpango wa kuamsha makali yake katika ngazi ya juu baada ya kuwa na msimu mbovu pale Manchester United.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alifunga magoli tisa katika michezo kumi na saba ya msimu wa kwanza akiwa na Monaco lakini kampeni yake iliisha baada ya kukumbwa na majeraha yaliyomfanya akose kushiriki kombe la Dunia mwaka jana.

Baadae Falcao alijiunga na klabu ya Manchester United kwa mkopo siku ya mwisho ya dirisha la usajili mwaka jana lakini amefurukuta kufanya vema Old Trafford bila mafanikio yoyote, alifunga magoli 4 kwenye michezo 29 aliyoichezea klabu hiyo.

Kabla ya kujiunga na klabu ya Monaco, Falcao alitambulika kama mshambuliaji matata na hatari baada ya kufunga magoli 70 katika misimu miwili tu akiwa na klabu ya Atletico Madrid na kutupia magoli matatu "Hat-trick" kwenye mechi ya Super Cup mwaka 2012 dhidi ya Chelsea.

0 comments:

Post a Comment