JACKSON MARTINEZ ATIMKIA AC MILAN

Friday, 12 June 2015



Wakala wa mshambuliaji wa Porto Jackson Martinez ana matumaini kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia atajiunga na klabu ya AC Milan. Klabu hizo mbili zipo mbioni kufikia makubaliano juu ya mchezaji huyo, alifafanua wakala huyo.

Klabu ya AC Milan inatarajia kuanza kujijenga vema baada ya kumaliza nafasi ya 10 msimu uliomalizika wa Serie A, kutokana na bajeti kubwa iliyopatikana kutoka kwa uwekezaji wa mfanyabiashara wa Thailand Bee Taechaubol katika klabu hiyo.

Uhusiano wa Martinez kujiunga na klabu hiyo umeenea haraka kukiwa na uvumi kwamba klabu hiyo ina nia ya kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani Zlatan Ibrahimovic, na sasa wakala wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia ameisifia Milan kuwa ni klabu kubwa.

"Nina matumaini juu ya uhamisho wa Jackson kwenda Milan, lakini bado hatuna uhakika," Luiz Henrique Pompeo aliiambia EuroStadio. "Kuna uwezekano mkubwa uhamisho huo ukatimia, lakini bado hatupo kwenye hatua ya kuweka mambo wazi kwa sasa."

"Ninachoweza kusema kwa hakika ni kwamba Martinez ni mchezaji anayestahili klabu ya juu kama Milan yenye historia."

"Je, watalipia €35,000,000? ni swala la kuwauliza Milan, sio swala la upande wetu. Kuhusu mshahara, siwezi kujadili takwimu kwa sasa. Lakini bado hakuna makubaliano na mchezaji huyo."

Klabu ya Porto imepanga kupata faida kubwa kutokana na mauzo ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia ambaye alisaini klabuni hapo mwaka 2012 kwa dau la €9m kama mbadala wa washambuliaji Radamel Falcao na Hulk waliotimka klabuni hapo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amethibitisha ubora wake katika klabu hiyo ya Estadio do Dragao kwa kupachika magoli 92 katika michezo 133 aliyowachezea miamba hao wa Ureno.

0 comments:

Post a Comment