BALOTELLI MBIONI KUTIMKA ANFIELD

Thursday, 30 July 2015

Balotelli Yu Njiani Kuihama Liverpool

Klabu ya Bologna ya nchini Italia ina matumaini ya kumrejesha kwenye ligi ya Sirie A, mshambuliaji Super Mario Balotelli, ambaye ameonyesha kutoyafurahia maisha ya nchini England tangu aliposajiliwa msimu uliopita na klabu ya Liverpool.

Bologna imedhamiria kumsajili Balotelli, huku ikitambua fika klabu ya Sampdoria ipo katika mchakato wa kimazungumzo na viongozi wa Liverpool ili kufanikisha mipango ya usajili wa mshambuliaji huyo.

Uwepo wa klabu hizo mbili za nchini Italia, unaongeza ushawishi kwa mashabiki wa Balotelli kuamini kutakua na uwezekano kwa mchezaji wao kurejea nyumbani na kucheza soka lake kama ilivyo kawaida.



Hata hivyo msukumo wa kuuzwa kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, umeendelea kupata kasi baada ya kusajiliwa kwa Christian Benteke Liolo akitokea Aston Villa juma lililopita.

Washambuliaji wengine waliosajiliwa huko Anfield ni, Roberto Firmino pamoja na Danny Ings.

Tayari meneja wa Liverpool Brendan Rodgers alishaeleza hatma ya Balotelli mbele ya waandishi wa habari kwa kusisitiza kwamba mshambuliaji huyo kutoka nchini Italia ana maamuzi ya mwisho wa kubaki ama kuondoka klabuni hapo kwa kutumia uwezo wake binafsi.

Balotelli alisajiliwa na Liverpool akitokea AC Milan kwa ada ya usajili wa pauni milioni 16, na alitarajiwa kufanya mambo makubwa kufuatia kuondoka kwa Luis Suarez, lakini mambo yalikwenda tofauti na kujikuta akifunga mabao machache katika michezo 16 aliyocheza.

Ada ya usajili wa Balotelli kutoka Liverpool tayari imeshatajwa kuwa ni pauni milioni 7.

0 comments:

Post a Comment