MWANA WA MFALME ALI BIN AL HUSSEIN AMPINGA PLATINI

Thursday, 30 July 2015 0 comments



Aliyekua mgombea nafasi ya urais wa shirikisho la soka duniani FIFA, Ali bin Al Hussein amempinga rais wa shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, Michel Platini kwa kusema hafai kusimama katika kinyang’anyiro cha kujaza nafasi ya Sepp Blatter kwenye uchaguzi wa mwezi februari mwakani.

Ali bin Al Hussein ambaye ni mtoto wa mfalme wa Jordan, ametoa angalizo hilo baada ya saa 24 kupita, ambazo zilishuhudia Platini akitangaza nia ya kuwania kiti cha uraisi wa FIFA baada ya kupata Baraka kutoka kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya UEFA mwishoni mwa juma lililopita.

Al Hussein amesema Platini hana sifa zilizo thabiti za kuiongoza FIFA ambayo kwa sasa imetapakaa uchafu wa rushwa, hivyo amewataka wadau wa soka duniani kutambua kwamba kuna ulazima kwa baadhi ya viongozi kujipima kabla ya kutangaza nia ya kuwania nafasi kubwa katika taasisi za kidunia.

Hata hivyo Al Hussein hakuweka wazi ni vipi Platini hatoshi katika nafasi hiyo kwa vigezo vya kuzuia rushwa, zaidi ya kusisitiza kuna ulazima kwa baadhi ya watu kujichunguza kwanza kutokana na vitendo vinavyoendelea miongoni mwa watu wanaowazunguuka.

Katika hatua nyingine Al Hussein, bado hajatangaza kama atawania nafasi ya urais kwa mara nyingine tena ama la, hali ambayo inahisiwa huenda ikawa ni hofu kwake baada ya kuona Platini ametangaza nia ya kukitaka kiti cha urais wa FIFA.

BALOTELLI MBIONI KUTIMKA ANFIELD

0 comments

Balotelli Yu Njiani Kuihama Liverpool

Klabu ya Bologna ya nchini Italia ina matumaini ya kumrejesha kwenye ligi ya Sirie A, mshambuliaji Super Mario Balotelli, ambaye ameonyesha kutoyafurahia maisha ya nchini England tangu aliposajiliwa msimu uliopita na klabu ya Liverpool.

Bologna imedhamiria kumsajili Balotelli, huku ikitambua fika klabu ya Sampdoria ipo katika mchakato wa kimazungumzo na viongozi wa Liverpool ili kufanikisha mipango ya usajili wa mshambuliaji huyo.

Uwepo wa klabu hizo mbili za nchini Italia, unaongeza ushawishi kwa mashabiki wa Balotelli kuamini kutakua na uwezekano kwa mchezaji wao kurejea nyumbani na kucheza soka lake kama ilivyo kawaida.



Hata hivyo msukumo wa kuuzwa kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, umeendelea kupata kasi baada ya kusajiliwa kwa Christian Benteke Liolo akitokea Aston Villa juma lililopita.

Washambuliaji wengine waliosajiliwa huko Anfield ni, Roberto Firmino pamoja na Danny Ings.

Tayari meneja wa Liverpool Brendan Rodgers alishaeleza hatma ya Balotelli mbele ya waandishi wa habari kwa kusisitiza kwamba mshambuliaji huyo kutoka nchini Italia ana maamuzi ya mwisho wa kubaki ama kuondoka klabuni hapo kwa kutumia uwezo wake binafsi.

Balotelli alisajiliwa na Liverpool akitokea AC Milan kwa ada ya usajili wa pauni milioni 16, na alitarajiwa kufanya mambo makubwa kufuatia kuondoka kwa Luis Suarez, lakini mambo yalikwenda tofauti na kujikuta akifunga mabao machache katika michezo 16 aliyocheza.

Ada ya usajili wa Balotelli kutoka Liverpool tayari imeshatajwa kuwa ni pauni milioni 7.

BENITEZ: SINA MUDA WA KUMJIBU MPUUZI MOURINHO

0 comments



Meneja wa klabu ya Real Madrid, Rafael Benitez amekataa kumjibu Jose Mourinho baada ya kurushiwa vijembe vilivyogusa maisha yake kisoka pamoja na familia.

Benitez, ambaye kwa sasa yupo mashariki ya mbali (China) sambamba na kikosi chake ambacho kinajiandaa na msimu mpya wa ligi, hakujibu jambo lolote pale alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya vijembe alivyorushiwa na Mourinho.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania, amesema yeye ni mwanasoka na katu hawezi kuyapa nafasi mazingira ya kipuuzi ambayo yamekua yakitengenezwa na watu wachache, kwa kujitafutia umaarufu duniani.

Amesema kwa sasa ni wakati mzuri kwake kuendelea na harakati za kukiandaa kikosi cha Real Madrid kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya AC Milan ambao utamsaidia kwenye mipango yake ya kufikia lengo la kufanya vyema msimu ujao wa ligi.



Chokochoko dhidi ya Benitez, zimechagizwa na kauli ya mke wa meneja huyo wa Real Madrid, Montserrat Seara, baada ya kusisitiza mara zote mume wake amekuwa akifanya vyema pale Mourinho alipopita huku akitolea mifano ya timu za Inter, Chelsea na sasa The Galacticos.

Kufuatia msisitizo huo Jose Mourinho hakuwa nyuma badala yake aliamua kurudisha mashambulizi kwa kusema maneno ya kashfa.

Mourinho aliwambia waandishi wa habari akiwa nchini Marekani kwamba, anahisi mke wa Benitez atakuwa amechanganyikiwa kwa namna fulani, kwa sababu mume wake alienda Chelsea kumrithi, Roberto Di Matteo na pia ameenda Real Madrid kumrithi Carlo Ancelotti.

Alisema kazi ambayo Benitez aliirithi kutoka kwake ni Inter Milan pekee, ambapo kwa takribani muda wa miezi sita tu alikiharibu kikosi ambacho kilikuwa bora barani Ulaya kwa kipindi hicho.

Mourinho aliongeza maneno yake kwa kumshauri mke wa Benitez kwa kumtaka aache kuzungumza kumuhusu yeye, kwani anahitaji kuutumia muda wake vizuri kufikiria diet (Mpangilio wa vyakula) ya mumuwe.

PSG YAICHAICHAPA MAN UNITED MBILI BILA...

0 comments



Mashetani wekundu Man Utd, wameshindwa kufurukuta mbele ya mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG, baada ya kutandikwa bakora mbili kwa sifuri katika mchezo wa kujiandaa na msimu mpya wa ligi.

Man Utd ambao wamekua na mazingira mazuri ya kupata ushindi katika michezo yao ya kirafiki iliyopita, iliyochezwa huko nchini Marekani walijikuta wakilamba kisago hicho kufuatia uwezo mzuri ulioonyeshwa na wapinzani wao kutoka Ufaransa.

Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic aliifungia PSG bao la pili katika dakika ya 34, baada ya kiungo kutoka nchini Ufaransa, Blaise Matuidi kufunga bao la kwanza katika dakika ya 25.

Katika mchezo huo mlinda mlango wa Man Utd, David De Gea alionekana kucheza chini ya kiwango na kocha wa Man Utd, Louis van Gaal alimtoa baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Kutokana na hali hiyo, Van Gaal sasa anawaza mawili, amruhusu aende Real Madrid au ampe mkataba mwingine, lakini kizungumkuti kingine kinachomkabili meneja huyo kutoka nchini Uholanzi ni kuamini De Gea ana mtazamo chanya (uzoefu) katika kikosi chake kwa sasa.

David De Gea amekuwa akihusishwa sana kuhamia Real Madrid, ingawa uongozi wa Man Utd umekua ukiweka msimamo wa kutomruhusu kuondoka.

Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya PSG umekua wa mwisho kwa mabingwa hao wa kihistoria katika soka la nchini England, na sasa watarejea nyumbani kumalizia sehemu ya maandalizi kabla ya kuanza kwa ligi mwishoni mwa juma lijalo.

Manchester United wataanza kurusha karata yao ya kwanza katika ligi ya nchini England dhidi ya Tottenham mnamo Agosti 8 mwaka huu.

HAZARD NI BORA KULIKO RONALDO-MOURINHO

Tuesday, 28 July 2015 0 comments




Meneja wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amempiga dongo mshambuliaji kutoka nchini Ureno pamoja na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo kwa kumtofautisha na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji, Eden Hazard.

Mourinho ambaye yupo njiani kurejea nchini England sanjari na kikosi chake akitokea nchini Marekani walipokua wameweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi, amesema Hazard ni mchezaji bora zaidi kuliko Ronaldo kutokana na uchunguzi wake alioufanya.

Meneja huyo kutoka nchini Ureno amesisitiza kuwa na uhakika wa jambo hilo ambalo alilizungumza mbele ya waandishi wa habari huko nchini Marekani huku akimuweka Ronaldo katika nafasi ya tatu kwa ubora duniani.

Alisema kwa soka la sasa ni vigumu kumfananisha Ronaldo na Hazard, hasa ikizingatiwa kiungo huyo wa klabu ya Chelsea msimu uliopita alikua lulu kwenye kikosi chake hadi kufikia hatua ya kutajwa kama mchezaji bora wa mwaka huko nchini England.

Mourinho, alikamilisha kwa kubainisha kwamba endapo akipewa nafasi ya kutaja walio bora duniani kwa sasa mchezaji wa kwanza kwake atakua Lionel Messi, kisha Eden Hazard halafu Ronaldo atafuatia.

Hata hivyo imekua ikiripotiwa kwamba Mourinho amekua hana mahusiano mazuri na Ronaldo wanapokua nje ya uwanja licha ya kuwahi kufanya kazi kwa pamoja huko mjini Madrid wakati meneja huyo alipokua mkuu wa benchi la ufundi la Real madrid.

Kabla ya Mourinho kwenda kukinoa kikosi cha Real Madrid, mara kadhaa aliwahi kumchokonoa Ronaldo kupitia vyombo vya habari lakini mshambuliaji huyo hakumjibu chochote zaidi ya kuendelea na shughuli zake za kucheza soka.

MAN CITY WAWASUMBUA VICHWA MABOSI WA FC BAYERN MUNICH..

0 comments



Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wanajipanga kufanya mazungumzo na Pep Guardiola, ili kukamilisha azma ya kumsainisha mkataba mpya wa kuendelea kukinoa kikosi cha klabu hiyo kwa miaka mingine ijayo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Munich, Karl-Heinz Rummenigge amethibitisha kufanyika kwa mipango ya kumsainisha mkataba mpya meneja huyo kutoka nchini Hispania na ana uhakika itakamilika.

Mkataba wa sasa wa Guardiola, unatafikia kikomo mwishoni mwa msimu ujao wa ligi, hali ambayo inazusha hofu miongoni mwa viongozi wa FC Bayern Munich kwa kuhisi huenda klabu nyingine duniani zikaanza kumnyatia.

Juma lililopita Rummenigge, alizungumza na kituo cha televisheni cha BeIN Sports na kueleza kwa uchache juu ya mipango hiyo, lakini hakutaka kuweka wazi ni vipi walivyojipanga kwa ajili ya kumshawishi Guardiola ili akubali kusaini mkataba mpya.

Klabu ya Man city ya nchini England, imekua ikitajwa sana kumuwania meneja huyo, hali ambayo inahisiwa huenda imekua msukumo kwa viongozi wa Bayern Munich kuanza mapema mchakato wa kutaka kumsainisha mkataba mpya.

Hata hivyo Pep Guardiola aliwahi kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza wazi mustakabali wake ndani ya FC Bayernm Munich na alisema ana matarajio ya kupanga mbivu na mbichi ndani ya mwaka huu.

Guardiola alipokea kijiti cha umeneja klabuni hapo kutoka kwa Jupp Heynckes, na amekua na mafanikio makubwa tangu alipokubali kufanya kazi na klabu hiyo mwaka 2013.

RAMOS NA PEREZ MAMBO SAFI KABISA...

0 comments



Rais wa klabu ya Real Madrid, Florentino Pérez Rodríguez amefanikiwa kufanya mazungumzo na beki wa kati kutoka nchini Hispania, Sergio Ramos García ambaye alikua mbioni kuihama klabu hiyo kutokana na sakata la kupewa mkataba ambao hakuridhishwa nao.

Perez, alilazimika kusafiri hadi nchini China mwishoni mwa juma lililopita kwa ajili ya kufanya mazungumzo na beki huyo, na taarifa zinadai kwamba tayari wawili hao wameelewana na wakati wowote Ramos atasaini mkataba mnono ambao utaendelea kumuweka Estadio Santiago Bernabeu.

Taarifa zinasema kwamba mkataba mpya ulioandaliwa na uongozi wa klabu ya Real Madrid, dhidi ya beki huyo mwenye umri wa miaka 29 utajumuisha donge nono la Pauni milioni 10 ambalo ni sawa na Euro milioni 13.5 ambazo zitamuwezesha kulipwa mshahara wake wa pauni 260,000 kwa juma.

JEZI MPYA ZA KILABU CHA SIMBA KUPATIKANA MTANDAONI

0 comments




Klabu ya Simba kwa kushirikiana na mtandao wa Jumia wamezindua huduma ya kununua jezi za Simba 2015 – 2016 kupitia duka la mtandao la Jumia www.jumia.co.tz .

Dhumuni la huduma hii ni kuwapatia wapenzi wa klabu ya Simba njia bora ya kuweza kununua jezi popote walipo Tanzania.

Kupitia mtandao imara na wenye uzoefu wa Jumia, klabu ya Simba inapanga kuongeza upatikanaji wa vifaa vyake vya michezo nchi nzima.

Mkataba huu utaongeza usambazaji wa vifaa vya michezo vya klabu ya Simba.

“Ukuaji wa kasi wa upatikanaji wa internet (mtandao) klabu ya Simba inafahamu umuhimu wa kuvifanya vifaa vyake vya michezo kuweza kupatikana kiurahisi kwa wateja wake, hivyo leo tunajivunia kuzindua huduma hii ya Jumia – Simba Online Shop kwa ajili ya kutumia mtandao wa Jumia kuwezesha wapenzi wa Simba popote walipo kuweza kununua mavazi na bidhaa za Simba kiurahisi na kwa bei nafuu”. Alisema Rais wa Simba Evans Aveva.



Maneja wa Jumia nchini Tanzania Jean –Philippe Boul aliongeza kwa kusema “Uzinduzi wa jezi za mpira wa miguu siku zote ni tukio muhimu kwenye maisha ya klabu maarufu na inayopendwa kama Simba.

Katika msimu wa 2015 – 2016 klabu ya Simba imeamua kuwa wabunifu kwa kutoa fursa kwa wapenzi wake kununua jezi za msimu 2015 – 2016 kupitia njia ya mtandao.

Tunajivunia sana kwa Rais wa Simba Evans Aveva kutuchagua Jumia kwa kazi hii. Kupitia huu umoja wetu wa Simba na Jumia tumeamua kutoa ofa kwa wanachama na wapenzi wa Simba kuagiza jezi kuanzia Jumatatu tarehe 27 – 7 – 2015 (jana) mpaka Alhamisi 31 – 7 – 2015 kupitia www.jumia.co.tz kabla ya kuanza rasmi kwa mauzo ya kimtandao kupitia Jumia na kuanza kuuzwa rasmi kwa rejareja”.

“Tunawahamasisha wapenzi wa Simba popote walipo Tanzania kuagiza jezi kupitia www.jumia.co.tz kuona urahisi katika kufanya manunuzi.

Popote walipo wapenzi wa Simba wanaweza kuagiza jezi kupitia tovuti ya jumia na kuletewa mzigo wako mpaka mlangoni.

Jumia pia inatoa njia tofauti za ulipaji kama vile kuweza kulipia pindi mzigo wako utakapofika au kufanya malipo kwa njia za kipesa kupitia simu za mkononi. Kuanzia jumatatu 27 – 7 – 2015 wapenzi wa Simba watapata fursa ya kuagiza jezi kupitia www.jumia.co.tz”. Aliongeza Maneja wa Jumia nchini Tanzania Jean –Philippe Boul.

Kuzungumzia mapinduzi haya makubwa katika usambazaji wa vifaa vya michezo vya klabu ya Simba Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya EAGgroup Limited Imani Kajula ambao ni washauri na watekelezaji wa masuala ya kibiashara wa klabu ya Simba alisema “Kwa mapinduzi haya makubwa yataiwezesha klabu ya Simba kuongeza mapato yake pia kudhibiti bidhaa feki, kupitia Jumia Online Shops (duka la mtandao la Jumia) wapenzi wa Simba watanunua bidhaa za Simba kupitia washirika halali wa uuzaji wa bidhaa za Simba Tanzania.

BLATTER ANASTAHILI TUZO YA NOBEL-PUTIN

0 comments



Rais wa Urusi Vladimir Putin ameshangazwa na lawama zinazoendelea kuelekezwa kwa rais wa FIFA Sepp Blatter, kufuatia sakata la mlungula linalowahusu baadhi ya maafisa wa shirikisho hilo la soka duniani kote.

Putin, ambaye nchi yake itakua mwenyeji wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, amesema haoni sababu za wadau wa soka duniani kuendelea kumuangushia lawama mzee huyo kutoka nchini Uswisi, kutokana na mambo mazuri ambayo ameyafanya duniani katika mchezo wa soka.

Putin, amesema Blatter ni msafi kati ya watu wasafi duniani na anastahili kutunukiwa tuzo ya Nobel, hivyo amewataka wadau wanaompinga kuacha mpango huo, na kufikiria ni vipi anavyousaidia mchezo wa soka duniani.

Sababu kubwa ya kiongozi huyo wa ngazi ya juu nchini Urusi, kujitokeza hadharani na kujaribu kumsafisha Blatter, imetajwa kuwa ni kuchoshwa na taarifa ambazo zimekua zikiendelea kuzungumzwa katika baadhi ya vyombo vya habari duniani, pamoja na kwa mtu mmoja mmoja kumuhusu kiongozi huyo wa FIFA.

Putin, amesisitiza kwamba, haiwezekani makosa ya watu wengine ndani ya FIFA yakawa mzigo kwa kiongozi wa shirikisho hilo ambapo mpaka sasa haijathibitika kama kweli alihusika na uchafu uliokua unafanywa na wasaidizi wake.

Kama itakumbukwa vyema shirika la upelelezi la nchini Marekani FBI, liliwakamata baadhi ya maafisa wa FIFA miezi miwili iliyopita huko nchini Uswisi baada ya kujiridhisha na ushahidi wa kuwepo kwa rushwa ndani ya shirikisho hilo.

Blatter, amekua sehemu ya upelelezi unaoendelea kufanywa na FBI na kama itabainika alihusika katika taratibu za kujihusisha na masuala ya rushwa kupitia shirikisho hilo atatiwa nguvuni.

UDIKTETA WA MOBUTU ULIVYOREJESHA MATUMAINI ANFIELD...

0 comments



Joseph-Desiré Mobutu alikuwa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka 1965 mpaka 1997. Aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Akajiita Mobutu Sese Seko na nchi akaiita Zaire. Alikuwa rais mashuhuri kwa udikteta uliopitiliza.
Jean-Pierre aliyekuwa askari wa jeshi la Zaire akaona aukimbie utawala wa mabavu wa dikteta Mobutu. Askari huyo akamchukua mke wake na mtoto wao mdogo wakahamia Ubelgiji mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mtoto akakulia Ubelgiji na akawa mwanasoka maarufu nchini Ubelgiji akicheza nafasi ya mshambuliaji.

Akazichezea klabu kubwa za Ubelgiji kama Standard Liège na Genk. Mwaka 2012 akahamia Aston Villa ya Uingereza kwa dau la paundi milioni 7 akitokea Genk. Huyo ni Christian Benteke. Wiki iliyopita alihamia Liverpool kwa dau la paundi milioni 32.5.
Anakuwa mchezaji ghali namba mbili kuwahi kusajiliwa na Liverpool baada ya Andy Carroll aliyasajiliwa kwa paundi milioni 35 akitokea Newcastle United 2011. Benteke ameifungia Aston Villa mabao 49 kwenye michezo 101 aliyoichezea. Usajili wake unapeleka matumaini Anfield. Huenda akainyanyua Liverpool.

Najaribu kujiuliza iwapo Benteke angepata nafasi ya kuichezea klabu kubwa kama Liverpool iwapo angekulia Kongo na kuiwakilisha bendera ya nchi hiyo. Mashaka yananijia nikiwatazama Trésor Mputu wa Kabuscorp SC ya Angola na Dioko Kaluyituka wa Al Gharafa ya Qatar.

Mputu akiwa nahodha wa TP Mazembe aliiwezesha kushinda kombe la Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo, 2009 na 2010. Akawemo kwenye orodha ya wachezaji watano waliowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika wa BBC 2009. Wengine wanne walikuwa Didier Drogba, Michael Essien, Samuel Eto’o, na Yaya Toure.

Kocha Claude Le Roy aliyekuwa kocha wa Cameroon kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998 aliwahi kusema kuwa Mputu ni Eto’o wa baadae. Rekodi, umahiri wa Mputu na sifa zote hizi hazikumwezesha kuchezea klabu yoyote ya Ulaya.
Dioko Kaluyituka pia ni mshambuliaji wa kiwango cha juu. Mwaka 2009 alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika alipofunga mabao 8 na kutwaa ubingwa akiwa na TP Mazembe.

Kwenye michuano ya Klabu Bingwa Dunia mwaka 2010 alifunga bao safi kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Internacional ya Brazil na kuipeleka Mazembe fainali. Akatwaa tuzo ya mpira wa fedha ‘silver ball’ kwenye michuano hiyo. Amewahi pia kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Qatar akifunga mabao 22 msimu wa 2013/14. Bado hakupata nafasi ya kucheza Ulaya.

Ninavyoona kinachowakwamisha Mputu na Kaluyituka ni kukulia Kongo na kuiwakilisha bendera ya nchi hiyo. Nchi ambayo imewahi kushiriki kombe la dunia mara moja tu 1974 na ikapoteza michezo yote. Ni taifa changa kisoka.

Mawakala wa soka la Ulaya, makocha na viongozi wa klabu wanaonekana kutokuwa na imani kuwa nchi kama hiyo inaweza kutoa wachezaji wa viwango vya juu. Naamini Mputu na Kaluyituka wangekulia Ubelgiji na kuiwakilisha bendera ya nchi hiyo kama Benteke nao wangepata nafasi ya kucheza soka katika moja ya klabu kubwa Ulaya.

Ubelgiji ina historia nzuri kwenye soka. Kwa sasa inashikilia nafasi ya tatu kwenye viwango vya ubora vya FIFA. Imeshiriki Kombe la Dunia mara 12. Inafahamika kwa kutoa wanasoka mashuhuri waliowahi kutamba Ulaya kama Fernand Goyvaerts, Luc Nilis, Vincent Kompany na wengine.

Kukulia Ubelgiji kumemfanya Benteke awe mchezaji mahiri. Pia bendera ya Ubelgiji imemfanya aaminiwe na klabu za Ulaya na hatimaye kuwa tumaini la Liverpool. Shukrani zimwendee dikteta Mobutu aliyefanya Benteke kuhamishiwa Ubelgiji akiwa mdogo. Pasingekuwepo dikteta huyu Benteke angeishia kuichezea Motema Pembe ya Kinshasa. Mobutu amepeleka matumaini Anfield.

"NITATIMKA MAN UTD, NIKATULIE NA MKE WANGU"-VAN GAAL...

0 comments



Meneja wa Manchester United Louis Van Gaal amesema kuwa huenda akaondoka katika kilabu cha Manchester United mwisho wa kandarasi yake ya miaka mitatu ili kutimiza ahadi alioitoa kwa mkewe.

Alipoulizwa iwapo ataongeza kandarasi yake katika uwanja wa Old Traford ,raia huyo wa Uholanzi ameiambia BBC kwamba ataondoka mwisho wa kandarasi yake mwaka 2017.

"Nilimuahidi mkewe wangu, hatuna miaka mingi iliosalia, na hiyo ndio sababu," alisema meneja huyo mwenye umri wa miaka 63.

"Nimefanya kila kitu katika maisha yangu kama mkufunzi." Alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wa yeye kusalia katika kilabu hicho, alijibu kwamba hawezi kutoa jibu lolote kwa kuwa mkewe amekasirika sana.

"Nakiri kwamba nilimwambia kuwa nitaastaafu ifikiapo miaka 55 lakini nikiwa na miaka 63 bado naendelea na ukufunzi na wiki ijayo nitakuwa na miaka 64," alisema meneja huyo.

WENGER: WALCOTT KUBAKIA ARSENAL, SCSZESNY KUJIUNGA NA ROMA KWA MKOPO...

0 comments



Mshambuliaji wa Arsenal, Theo Walcott anakaribia kuongeza mkataba wake na klabu hiyo hadi mwaka wa 2019.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amefichua kuwa Walcott atasaini kandarasi mpya na timu hiyo huku akiwa amesalia na mwaka mmoja tu katika klabu hiyo.

Walcott mwenye umri wa miaka 26 aliifungia Arsenal goli la kipekee dhidi ya Wolfsburg na kuiwezesha Arsenal kuondoka na kombe la Emirates.

Aidha, kipa wa Poland, Scszesny yuko mjini Roma, nchini Italia kujiunga na As Roma baada ya kupoteza nafasi yake kwa aliyekuwa kipa wa Chelsea, Petr Cech.



Scszesny anasubiri ukaguzi wa kimatibabu kabla ya kujiunga na timu hiyo kwa njia ya mkopo wa muda mrefu.

Meneja wa Arsenal, Wenger, amekuwa chini ya shinikizo kali kuimarisha timu hiyo ili kuleta ushindani mkali kwenye ligi ya Uingereza pamoja na ligi ya vilabu bingwa Ulaya msimu huu.
Arsenal inalenga kuondoka na taji la tatu kabla ya msimu kuanza itakapochuana na Chelsea uwanjani Wembley wikendi ijayo.

YANGA ITAFIKA FAINALI KAGAME, AJIGAMBA PLUIJM...

0 comments

Yanga itafika fainali Kagame, ajigamba Pluijm

Yanga imemaliza nafasi ya pili kwenye kundi lake la A lililokuwa na timu tano na Jumatano itacheza na ndugu zao Azam ukiwa ni mchezo wa robo fainali

KOCHA wa Yanga Hans van der Pluijm amesema anauhakika kikosi chake kitacheza fainali ya michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Pluijm ameiambia Goal ushindi wa bao 1-0 walioupata jioni ya jana dhidi ya Khartoum ya Sudan umedhihirisha ubora waliokuwa nao licha ya kuanza vibaya michuano hiyo kwa kufungwa na Gor Mahia kwenye mchezo wa ufungzi.

“Nafurahi kuona tumeanza kurudi kwenye ubora wetu baada ya kuanza vibaya kila mchezo tumekuwa tukibadilika na kiwango tulichokionyesha leo ni tofauti kabisa na kile tulichoonyesha kwenye mechi zetu tatu zilizopota na hii ni ishara kwamba tunataka ubingwa,’amesema Pluijm.

Yanga imemaliza nafasi ya pili kwenye kundi lake la A lililokuwa na timu tano na Jumatano itacheza na ndugu zao Azam ukiwa ni mchezo war obo fainali.

MAN UTD YAMSAJILI KIPA SERGIO ROMERO...

0 comments



Kipa Sergio Romero, aliyekuwa akiichezea klabu ya Sampdoria, amejiunga na vijana wa Louis Van Gaal baada ya kukamilisha muda wa mkataba wake na Sampdoria.

Romero aliwahi kucheza chini ya Van Gaal katika timu ya AZ Alkmaar ya Uholanzi iliyotwaa ubingwa wa kombe la ligi ya Uholanzi mnamo mwaka wa 2009.

Kipa huyo ametia saini mkataba wa miaka mitatu na anatarajiwa kuchukua nafasi ya kipa wa akiba, Victor Valdes ambaye ameambiwa yuko huru kuihama klabu hiyo na Van Gaal.
Romero alikuwa katika timu ya taifa ya Argentina iliyofika fainali ya Copa America mwaka huu na kombe la dunia nchini Brazil mwaka uliopita.

Kwa sasa kipa huyo ameungana na wana-devils katika kambi ya mazoezi ya timu hiyo nchini Marekani.

Mchezaji huyo ni miongoni mwa wachezaji waliofunzwa na Van Gaal ambao wameungana naye Old Trafford wengine wakiwa ni Memphis Depay, na Daley Blind.

Hatua ya kumsaini Romero inaonekana ni kama njia ya kupiga jeki idara ya ulinzi katika Manchester United huku Mhispania, David De Gea akiendelea kusakwa na Real Madrid.

JACKSON ARLEY MARTINEZ ATAMBULISHWA RASMI ATLETICO MADRID...

0 comments



Mshambuliaji kutoka nchini Colombia, Jackson Arley Martínez, anaamini kusajiliwa kwake kwenye kikosi cha Atletico Madrid ni hatua nzuri kwa klabu hiyo ya mjini Madrid, kurejesha heshima ya kutwaa tena ubingwa wa nchini Hispania msimu ujao wa ligi.

Martinez, alieleza matarajio hayo, wakati aliposalimiana na mashabiki 10,000 waliokua wamejitokeza kwenye uwanja wa Vicente Calderón, katika shughuli ya kutambulishwa.



Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amesema usajili wake anaamini utaongeza nguvu katika mipango ya klabu hiyo ya kuhakikisha wanarejesha heshima baada ya msimu uliopita kupokonywa ubingwa wa La Liga na FC Barcelona.

Hata hivyo amewataka mashabiki kuwa na uvumilivu pale mambo yatakapokwenda mrama katika msimu mpya wa ligi ya Hispania lakini akasisitiza wazi kwamba lengo ni mafanikio kwanza na mengine yatakayojitokeza katika safari yao yatachukuliwa kama majaribu.



Wakati wa shughuli ya kutambulishwa mbele ya mashabiki, baadhi ya makazi wa Atletico Madrid walishindwa kujizuia kwa furaha na kujikuta wakiruka uzio na kuingia kwenye sehemu ya kuchezea ili wakamilishe azma ya kumshika mshambuliaji huyo kitendo ambacho kilifanikiwa kabla ya maafisa wa usalama hawajawaondoa uwanjani.

Martinez, amejiunga na Atletico Madrid kwa usajili wa pauni milioni 25 akitokea FC Porto ya nchini Ureno.

TETESI ZA USAJILI: MAN U KUMREJESHA RONALDO OLD TRAFFORD, LEWANDOWSKI KUTUA ARSENAL KAMA WATAMKOSA BENZEMA...

Friday, 24 July 2015 0 comments

MANCHESTER UTD WANAJARIBU KUMSAJILI RONALDO:



Klabu ya Manchester United wanajaribu kumrejesha Old Trafford mchezaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo. Mashetani hao wekundu wana kazi ya kufanya dili ambalo litakuwa rekodi mpya klabuni hapo huku wakiwa na nia ya kusajili wachezaji wenye viwango vya juu majira haya.

Chanzo: Manchester Evening News
Alhamisi, 7/23/2015 20:05

PSG WAMEKUBALI ADA YA DI MARIA YENYE THAMANI YA EURO 65 MILIONI:



PSG wamekubaliana na Manchester United ada ya euro milioni 65 sawa na pauni milioni 45.5 kwa ajili ya kumsajili Angel Di Maria. Mchezaji huyo wa Kiargentina ataungana na wachezaji wenzake wa  timu yake mpya huko USA wikiendi hii.

Chanzo: France Football
Alhamisi, 7/23/2015 20:37

SAMPER AMEPANGA KUZUNGUMZA NA BARCA HUKU KUKIWA NA UVUMI TOKA KWA ARSENAL:



Sergi Samper anajipanga kuzungumza na klabu yake ya Barcelona kuhusiana na mustakabali wake huku kukiwa na uvumi kutoka katika kilabu cha Arsenal ambao wanamtazama mchezaji huyo kijana kama mbadala wa Mikel Arteta kilabuni hapo.

Chanzo: Daily Express
Alhamisi, 7/23/2015 19:37

WEST HAM NA EVERTON VINAMUWANIA HALILOVIC KWA MKOPO:



Barcelona wanatazamia kumruhusu Alen Halilovic kujiunga kwa mkopo huku wote Everton na West Ham wakimuwania mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19.

Chanzo: Daily Mail
Alhamisi, 7/23/2015 19:00

MADRID HAITOMUUZA RAMOS:



Raisi wa kilabu cha Real Madrid Florentino Perez atafanya mazungumzo na Sergio Ramos wikiendi hii na atamwambia beki huyo kuwa kilabu hicho hakitamuuza majira haya.

Chanzo: The Gurdian
Alhamisi, 7/23/2015 17:18

WELBECK KWENYE RADA YA BESIKTAS:



Besiktas wanatazamia kumnyatia mshambuliaji wa kilabu cha Arsenal Danny Welbeck.

Chanzo: Fanatik
Alhamisi, 7/23/2015 16:32

MADRID WATAMJUMUISHA NAVAS TU KWENYE DILI LA DE GEA:



Real Madrid wameimbia klabu ya Manchester United kuwa hawatolipa zaidi ya euro milioni 25 sawa na pauni milioni 17.6 kwa ajili ya kuipata saini ya David De Gea na watamjumuisha Keylor Navas tu kwenye dili hilo.

Chanzo: ABC
Alhamisi, 7/23/2015 15:45

NORWICH INAMUWANIA ALONSO:



Norwich City wanajiandaa kutoa kitita cha euro milioni 3 sawa na pauni milioni 2.1 kumnyakuwa mlinzi wa klabu ya Fiorentina  Marcos Alonso.

Chanzo: Mediaset
Alhamisi, 7/23/2015 15:00

PSG WAMETOA DAU KWA AJILI YA LACAZETTE:



Paris Saint-Germain wamewasilisha euro milioni 38 (pauni milioni 26.8) kwa ajili ya kumnyakuwa mshambuliaji wa Lyon Alexandre Lacazette.

Chanzo: Gazzetta dello Sport
Alhamisi, 7/23/2015 14:57

WEST BROM KWENYE MAZUNGUMZO NA DIABY:



West Brom wapo kwenye mazungumzo na kiungo wa zamani wa Arsenal Abou Diaby.

Chanzo: Birmingham Mail
Alhamisi, 7/23/2015 13:44

TOTTENHAM, WEST HAM NA ASTON VILLA KWENYE VITA YA BOLASIE:



Tottenham, West Ham na Aston Villa wote wameulizia upatikanaji wa nyota wa Crystal Palace Yannick Bolasie na The Eagles hao wanatarajia kupokea dau angalau kutoka katika vilabu viwili kwa ajili ya winga huyo.

Chanzo: Sky Sports
Alhamisi, 7/23/2015 12:25

LIVERPOOL WAMRUDIA PEDRO:



Huku Manchester United wakiwa katika mbio za kumnyakuwa Pedro, Liverpool wameingia tena kwenye mbio hizo za kumsajili mchezaji huyo kutoka Barcelona.

Chanzo: Mundo Deportivo
Alhamisi, 7/23/2015 11:13

LAZIO WAMEKATAA DAU LA MAN UTD KWA BIGLIA:



Lazio wamekataa dau la euro milioni 25 (pauni milioni 17.5) lililotolewa na kilabu cha Manchester United kwa ajili ya kumpata Lucas Biglia.

Chanzo: Corriere dello Sport
Alhamisi, 7/23/2015 10:24

ARSENAL WANAANDAA DAU LA ISCO:



Arsenal wapo tayari kutoa ofa kwa nyota wa Real Madrid Isco. Mchezaji huyo wa Kihispania amepambana kujipatia namba Bernabeu na inaweza kumfanya atimke klabuni hapo, huku Arsene Wenger akitazamia kuiba kile Chelsea na Man City wakitazamia.

Chanzo: Daily Star
Alhamisi, 7/23/2015 09:48

CHELSEA WANAFANYA MAZUNGUMZO NA CALLEJON:



Chelsea wanatarajia kumnyatia mchezaji wa Napoli Jose Callejon na wamefungua mazungumzo na timu hiyo ya Italia. Maurizio Sarri yupo tayari kumuondoa mchezaji huyo wa Hispania, amabaye atagharimu pauni milioni 10.4, na wanatumaini kumleta Mohamed Salah kama sehemu ya dili hilo.

Chanzo: Metro
Alhamisi, 7/23/2015 09:44

VARANE KUMFANYA RAMOS KUBAKI MADRID:



Real Madrid wameamua kumbakiza klabuni hapo beki wao wa kati Sergio Ramos kutokana na hali ya Raphael Varane kutokuwa fiti. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ana matatizo ya goti ya muda mrefu, yaliyomfanya akose mazoezi msimu uliopita, kwa hiyo Ramos hatoruhusiwa kutimka klabuni hapo.

Chanzo: El Confidencial
Alhamisi, 7/23/2015 09:27

ARSENAL INAMNYEMELEA LEWANDOWSKI:



Arsenal wapo tayari kudondosha sarafu yao kwa mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski kama dili la kumnyakuwa Karim Benzema litashindikana. Arsene Wenger anajaribu kumleta nyota huyo wa Real Madrid, lakini anatazamia kuwa raia huyo wa Poland kuwa mbadala wa dili hilo.

Chanzo: Metro
Alhamisi, 7/23/2015 09:26

INTER WANATARAJIA KUMSAJILI JOVETIC:



Inter wamefikia makubaliano na klabu ya Manchester City juu ya uhamisho wa Stevan Jovetic kwa dili la miaka miwili ya mwanzo ya mkopo, pamoja na kuwa na wajibu wa kumnyakuwa moja kwa moja kwa ada ya euro milioni 20.

Chanzo: Corriere dello Sport
Alhamisi, 7/23/2015 07:29

TETESI ZA USAJILI: MAN UTD KUTOA EURO 100M KWA MULLER, MOUTINHO ARUHUSIWA KUJIUNGA NA ARSENAL...

Thursday, 23 July 2015 0 comments

MAN UTD KUTOA EURO MILIONI 100 KWA MULLER:



Mshambuliaji wa 'siri' wa Louis van Gaal ni Thomas Muller. United wapo tayari kutoa dau la euro milioni 100 kumpata nyota huyo wa Bayern Munich.

Chanzo: Bird
Jumatano, 7/22/2015 08:01

MOUTINHO YUPO HURU KUJIUNGA NA ARSENAL:



Mchezaji wa kimataifa wa Ureno Joao Moutinho ameambiwa na klabu yake ya Monaco kwamba yupo huru kufanya mazungumzo ya kuhamia Arsenal. The Gunners wamekuwa wakihusishwa na kuwa na nia kubwa juu ya kiungo huyo na yupo huru kufanya makubaliano kuhamia Londoni kaskazini.

Chanzo: Daily Star
Jumatano, 7/22/2015 15:56

ARSENAL WANAKARIBIA KUMCHUKUA KIUNGO WA BARCA:



Arsenal wanajiandaa kumnyakuwa kiungo wa Barcelona Sergi Samper na wamejipanga kufikia bei ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20. Arsenal Wenger amemuelezea mchezaji huyo kinda kuwa ndiye mrithi wa Mikel Arteta na yupo tayari kutoa dau la pauni milioni 8.4.

Chanzo: Metro
Jumatano, 7/22/2015 10:23

WEST HAM INAMTAKA CAMBIASSO:



West Ham wapo tayari kumnyakuwa Esteban Cambiasso baada ya kiungo huyo kugoma kuongeza mkataba katika klabu ya Leceister City. The Hammers wanapambana na Barca kukubaliana dili la kumsajili Alex Song na badala yake huenda wakaelekeza mawazo yao kwa mkongwe huyo wa Argentina.

Chanzo: Evening Standard
Jumatano, 7/22/2015 11:36

LIVERPOOL INAMUWINDA DIGNE:



Liverpool imeelekeza sarafu yake kwa mlinzi wa Paris Saint Germain Lucas Digne. Baada ya Christian Benteke kukamilisha usajili wa saba katika klabu hiyo, Brendan Rorgers bado anataka beki wa kushoto, iwe kwa mkopo au kwa dili la kudumu.

Chanzo: Daily Mirror
Jumatano, 7/22/2015 11:32

DILI LA PERISIC KWENDA INTER LIMEKAMILIKA KWA DAU LA EURO MILIONI 18:



Inter Milan na Wolfsburg wamefikia makubaliano kuhusu uhamishao wa Ivan Perisic. Mshambuliaji huyo raia wa Croatia ataigharimu Inter ada ya euro milioni 18.

Chanzo: Corriere dello Sport
Jumatano, 7/22/2015 09:17

PEREZ ANAJIPANGA KUZUNGUMZA NA RAMOS:



Florentino Perez anajipanga kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Sergio Ramos huko China. Raisi huyo wa Real Madrid atahudhuria Guangzhou na Shanghai kutazama michezo yao ya maandalizi ya msimu na amepanga kujadiliana na beki huyo kuhusu muafaka wake kilabuni hapo.

Chanzo: AS
Jumatano, 7/22/2015 23:49

ASTON VILLA INAMUWANIA ROLAN:



Aston Villa inamuwania Diego Rolan kuchukua nafasi ya Christian Benteke ambaye ametimkia katika klabu ya Liverpool . Newcastle imevutiwa pia, lakini Bordeaux  wanataka euro milioni 20 kwa ajili ya mshambuliaji huyo.

Chanzo: Sud Ouest
Jumatano, 7/22/2015 06:56

MCHEKESHAJI ALIYEMKASHIFU BLATTER KUKIONA CHA MOTO, AFUNGULIWA MASHITAKA...

Wednesday, 22 July 2015 0 comments



Mchekeshaji kutoka nchini Uingereza Simon Brodkin, aliyevamia mkutano wa rais wa shirikisho la soka duniani (FIFA) Sepp Blatter wakati akuzungumza na waandishi wa habari mwanzoni mwa juma hili atafunguliwa mashitaka kufuatia kitendo hicho.

Mamlaka ya jeshi la polisi nchini Uswisi, imethibitisha taarifa za kufunguliwa mashitaka kwa mchekeshaji huyo, kwa kosa la kuvamia mkutano wa rais wa FIFA bila kibali maalumu hasa ikizingatiwa hakuwa na sifa za uandishi wa habari kama ilivyokua kwa wageni waalikwa kutoka katika vyombo vya habari.



Taarifa zinasema kwamba mchekeshaji huyo alionesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu, baada ya kumrushia pesa bandia rais wa FIFA Sepp Blatter, hali ambayo imeongeza kichocheo cha kufunguliwa mashitaka akiwa nchini Uswisi.

Hata hivyo alipopanda jukwaani mchekeshaji huyo alijitambulisha kwa jina la Lee Nelson, hatua ambayo bado inaendelea kudhihirisha alikua muongo na hakua na dhamira njema katika mkutano huo.

Simon Brodkin, mwenye umri wa miaka 38, amekua akifanya matukio mbali mbali ya kuvamia mahala pasipomuhusu, kwani aliwahi kujichanganya na wachezaji wa timu ya taifa ya Uingereza wakati wakijiandaa kusafiri kuelekea nchini Brazil kwa ajili ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, pia aliwahi kupanda jukwani wakati msanii wa muziki kutoka nchini Marekani Kanye West akitumbuiza jijini Londoni.